Love stories
LAITI KAMA NINGEKUFAHAMU KABLA.........HADITHI YA KUFIKIRIKA
Miaka
mitano iliyopita nilikuwa natafuta mke wa kumuoa ambaye angekuwa na
sifa nizitakazo. Nilikuwa natafuta msichana mzuri wa wastani maana
sikutaka kuoa mke mzuri kupindukia asije niua bure kwa presha na
jakamoyo. Nilikuwa natafuta binti atakanikubali kama nilivyo na
mapungufu yangu na mimi niliahidi kumkubali na mapungufu yake ili mradi
asiwe ni mwenye tamaa ya kupenda sana pesa na mfujaji. Awe na staha na
anayeweza kukabiliana na hali yoyote, niwe nacho, nisiwe nacho au kwa
kifupi tupendane kwa shida na raha. Pamoja na sifa nyingine ndogo ndogo,
lakini muhimu ni upendo na amani vitawale nyumbani kwangu. Hatimaye
nilimpata Binti Yasinaty, na kukutana kwetu kulikuwa ni kama muujiza,
nakumbuka siku hiyo nilipanda daladala nikielekea kazini na kwa bahati
kiti nilichokalia kilikuwa ni cha mwisho upande wa dirishani. Wakati
nakaa nikahisi kukalia kitu kigumu, nilipopapasa ilikuwa ni simu mpya
kabisa tena ya bei mbaya kama sikosei wakati huo ilikuwa inauzwa
shilingi laki nne kwa wakati huo, kumbuka kwamba hapa nazungumzia habari
ya miaka mitano iliyopita. Kwa bahati mbaya simu ile ilikuwa imezimwa,
na nilipojaribu kuiwasha iliwaka na kuzima kuashiria kwamba betri yake
iliisha chaji. Niliiweka mfukoni na kujiuliza kuwa ile simu ilikuwa ni
ya nani, sikusikia mtu kulalamika kwamba amepoteza simu na niliogopa
kuuliza maana nilichelea mtu kujitokeza na kusema kwamba ni yake ilihali
sio ya kwake. Nilifika ofisini na kuanza kazi, baadae nilimuita katibu
muhtasi wangu na kumwomba anisaidie kutafuta chaji ya ile simu kwa
kuwauliza wafanyakazi pale ofisini, nilikuwa na shauku ya kumfahamu
mwenye simu ile ili nimrudishie, kwani nilikuwa namuoana dhahiri
akisikitika kwa kupotelewa na simu yake, kwa jinsi ilivyoonekana ilikuwa
bado ilikuwa ni mpya kabisa na ilikuwa haijatumika zaidi ya wiki.
Katibu wangu muhtasi hakufanikiwa kuipata ile chaja ya ile simu.
Niliweka ile simu kwenye droo ya ofisini kwangu ili jioni nikitoka
nipitie nayo kariakoo ninunue chaja yake.Ilipofika jioni alikuja mchumba
wangu ambaye tulitofautiana wiki iliyopita na kuamua kutengana naye.
Sikutaka kuonana naye na nilimwambia katibu wangu muhtasi amwambie kuwa
niko bize na sitaki afike tena pale ofisini kwangu. Ukweli ni kwamba
nilimpenda sana lakini kitendo chake cha kukuta mwanaume mwingine
chumbani kwake tena akiwa amelala kitandani kwake halafu anajidai
kunidanganya kuwa eti ni binamu yake hakikunifurahisha kabisa. Nakumbuka
nilisafiri kikazi kwenda Mbeya, na ilikuwa nikae kule kwa wiki moja,
lakini ilitokea dharura huku Makao makuu Dar ikabidi nirudi baada ya
siku mbili tu na nilipofika kwa kuwa ilikuwa ni usiku kama saa mbili
niliamua kupitia kwa mchumba wangu ambaye alikuwa akiishi Mwenge ili
kupata chakula cha jioni kabla sijaenda kwangu Maeneo ya Sinza.
Nilipofika nilimkuta akiwa nje akipika, lakini aliponiona alishtuka sana
akabaki kinywa wazi, hakunipokea alibaki ameduwaa, nikahisi kuna jambo.
Nilimsalimia alijibu kwa wasiwasi nilipotaka kuingia ndani, alinizuia,
na huku akiongea kwa sauti yenye kutetemeka aliniambia eti ndani kuna
binamu yake kaja na amejipumzisha kitandani kwake, nilishtuka.
Niliiingia ndani moja kwa moja na kumkuta kijana amelala kitandani
nilipomuhoji kuwa yeye ni nani na anafanya nini pale akaniambia kuwa
yuko pale kwa girlfriend wake na alitaka kujua eti mimi ni nani.
Sikutaka kuzua ugomvi, nilimwambia kuwa pale ni kwa dada yangu na
nilifika kumsalimia, nilimuomba radhi kwa kuingia bila hodi, ila
nilimshauri aharakishe kulipa mahari ili tujue kuwa dada yetu anaye mtu,
ili wakati mwingine tubishe hodi, niliongea kwa utani, yule kijana
alimsifia sana mchumba wangu kuwa ni mzuri hasa na anajua kupenda,
alibwabwaja mambo mengi na upuuzi wao wanaofanya nikiwa sipo, niliongea
naye kwa utani mwingi na kuaga na kuondoka, lakini moyoni roho ilikuwa
ikiniuma kweli. Nilikuwa nampa yule binti karibu kila kitu alichohitaji,
lakini kumbe hakuridhika bado akawa na mwanaume mwingine.Nilitoka na
nilimkuta kajiinamia pale nje, sikumuaga nikaondoka zangu. Nilipofika
nyumbani nilimtumia ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani nikimwambia kuwa
kuanzia siku hiyo ilikuwa ni mwisho wa uhusiano wetu. Hakijibu na siku
iliyofuata alipiga simu lakini sikupokea, alibadilisha namba na
nilipopokea na kugundua kuwa ni yeye nilikata simu, baadae zilifuata
ujumbe kadhaa wa simu yake ya kiganjani akitaka tuonane ili tuyamalize.
Sikumjibu. Na ndio akaamua kuja ofisini. Nilimpigia simu katibu muhtasi
wangu na kumuamuru amwambie yule binti aondoke pale ofisini. Niliambiwa
kuwa amekataa, nilimpigia simu dereva wangu na kumuuliza kama gari
limeshatoka gereji, akanijibu kuwa gari litatoka baadae kidogo,
nikamwambia akitoka gereji aende nalo nyumbani kisha kesho asubuhi
anifuate. Gari langu liliharibika siku mbili zilizopita, hivyo
nililazimika kupanda daladala au taxi kama nikiwa na dharura. Niliondoka
pale ofisini nikimuacha akiongea na katibu wangu muhtasi na kuondoka
zangu. Nilikodi taxi na wakati niko njiani nikakumbuka kuhusu ile simu,
lakini niliisahau ofisini, kwa hiyo sikupitia kariakoo tena. Nilikwenda
moja kwa moja hadi kwa rafiki yangu anayeishi maeneo ya Kijitonyama na
kupoteza muda huko hadi usiku ndio nikarudi nyumbani. Siku iliyofuata
dereva alinifuata na kunipeleka ofisini, nilipofika nilimpa ile simu na
kumtuma akanitafutie chaja ya ile simu. Baadae alirudi akiwa na chaja ya
simu ile na kunikabidhi. Niliichaji na ilipojaa niliiwasha ziliingia
ujumbe kadhaa kutoka kwa watu waliokuwa wakimtafuta mwenye simu ile,
nilipozisoma niligundua mwenye simu ile alikuwa anaitwa Yasinaty,
nilikata shauri nimpigie mmoja wa watu waliokuwa wametuma ujumbe ambaye
alionekana kuwa ni mama yake. Nilipompigia simu na kuuliza kama anamjua
mwenye simu kwanza alitaka kujua mimi ni nani na kwa nini simu ya
mwanaye ninayo mimi. Nilimsimulia kila kitu na nilimuomba ampe mwanae
namba yangu ya simu na kumuomba amwambie awasiliane na mimi ili nimpe
simu yake. Yule mama alifurahi sana na kunishukuru sana, kumbe ile simu
Yasinaty alitumiwa na kaka yake aishie Ughaibuni. Mchana nilipigiwa simu
na Yasinaty na tuliongea mengi na alionekana ni binti mchangamfu kweli,
alinimbia kuwa anafanya kazi kwenye Hoteli moja ya kitalii maarufu
iliyoko katikati ya jiji, nilimuahidi kumpitia kazini kwake jioni
nikitoka ofisini. Nilimpitia jioni na kama alivyonielekeza kuwa yuko
reception nilimkuta pale akimalizia kazi na aliniomba nimsubiri kweye
kijimgahawa kilichopo pale ndani, kwa kuwa mimi sio mnywaji wa pombe
niliagiza juisi ili kumsubiri. Baadae alinipitia pale nilipokaa na
kunimbia kuwa anatoka hivyo tukutane nje kwani anakwenda kubadili sare
za kazini. Alitoka na kunikuta nje nikimsubiri, alipanda kwenye gari na
nilimuomba dereva wangu atupeleke Hoteli nyingine ya kitalii maarufu
pale hapa jijini ili tupate kahawa na Yasinaty. Tulifika pale tuliagiza
vinywaji. Nilitumia wasaa ule kumtazama vizuri Yasinaty, alikuwa ni
binti mrembo sana, na mchangamfu hasa, naamini alistahili kufanya kazi
reception. Nilimkabidhi simu yake na yakafuata maongezi mengine ya
kujuana na simulizi za hapa na pale. Huo ndio ukawa mwanzo wa kujuana na
Yasinaty, ambaye baadae alikuja kuwa mke wangu mpenzi. Laiti kama
ningekufahamu kabla Yasinaty………………….Habari hii nimetumiwa na msomaji wa
blog hii ya MAISHA NA MAFANIKIO ambaye anasheherekea ndoa yake kutimiza
miaka mitano leo. Na nimeona si vibaya kama nikiweka hapa kibarazani.
GUD STORY..
ReplyDelete