Sports



Msumbiji waja Ijumaa


Kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Msumbiji (Mambas) kinatarajia kutua nchini Ijumaa Julai 18 mwaka huu kwa ajili ya kuwakabili wenyeji timu ya Tanzania (Taifa Stars) katika mechi ya kwanza ya kuwania nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Mechi kati ya Stars na Mambas itafanyika Jumapili Julai 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam itachezwa kuanzia saa 12:00 jioni na timu hizo zitarudiana Agosti 3 mjini Maputo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Selestine Mwesigwa, alisema kuwa Msumbiji wametuma taarifa hiyo ya awali bila kutaja idadi ya wachezaji na viongozi watakaowasili siku hiyo.

Mwesigwa alisema pia waamuzi watakaochezesha mechi hiyo kutoka Misri na kamishna wa mchezo huo kutoka Zimbabwe wataingia jijini Jumamosi.

Katibu huyo alisema kuwa maandalizi mengine ya mchezo huo yanaendelea vizuri na tayari shirikisho limeshatuma tiketi kwa nyota watatu (Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu na Mwinyi Kazimoto) wanaocheza nje ya nchi ambao wameitwa na kocha wa Stars, Mholanzi Mart Nooij.

"Kila kitu kinakwenda vizuri na habari nzuri ni kwamba Samata na Ulimwengu wanaweza kujiunga mapema na timu tofauti na tulivyotarajia wawasili Jumatano," alisema Mwesigwa.

Alisema kwamba mechi tatu za kirafiki za kimataifa walizocheza zimelisaidia benchi la ufundi kuona mapungufu na kuyafanyia kazi ili waweze kufanya vizuri Jumapili.

Stars ilifuzu kucheza hatua ya pili katika kusaka tiketi ya kuelekea kwenye fainali zitakazofanyika mwakani Morocco baada ya kuifunga Zimbabwe mabao 3-2.

Mara ya mwisho Stars kushiriki fainali za AFCON ilikuwa ni mwaka 1980 na 2008 ilicheza fainali za kwanza za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani zilizofanyika Ivory Coast.

Chanzo:www.ippmedia.com